Usalama Wa Ikulu Ya Magogoni Ni Kudra Za Mungu Tu


Ikulu (State House) ya nchi ya Tanganyika sasa Tanzania lijengwa kwa namna ya kipekee na Wajerumani mwaka 1891 na gavana wa Kihuni Chakosi Dikwe na kutumika kama ngome ya gavana. Iliharibiwa wakati wa vita kuu ya kwanza ya dunia. Baada ya vita ya kwanza ya Dunia Tanganyika ilikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Waingereza na hapo ngome hiyo (state house) iliitwa Nyumba ya Serikali “Government House”na ilijengwa tena mwaka 1922. Majengo hayo yamejengwa kwa ubora wa pekee na ni ya kihistoria kwani yalikuwa ni Ngome za magavana. Eneo la ikulu hiyo lilikuwa na ukubwa wa ekari 30 likianzia barabara ya Ohio ilipo Mahakama ya Rufani mpaka Hospitali ya Aghakhan kuizunguka bahari. Makazi haya ya rais nchini Tanzania yaliko Kaskazini Mashariki mwa jiji la Dar katika nyuzi 2 kutoka usawa wa bahari ndio makazi ya kiongozi wa nchini yaliyohatarini zaidi kuliko makazi ya rais yeyote barani Afrika kwa sasa.

Ikulu ya Magogoni
Mageuzi ya dunia yametokea katika zama nzuri za karne 21, na dunia imewalazimisha watu kugeuka vile itakavyo. Katika uwanda wa kijasusi viongozi wa dunia walikuwa wanaondolewa kwa njia nyingi, kama kura, risasi ama sumu. Huo ndio msingi wa wa maisha ya ujasusi wa kidola duniani na nguvu ya ladha ya madaraka. Leo dunia imehama, ipo hapa ilipo na ujasusi wa kidola umehama, njia mpya za kumuondoa kiongozi yeyote madarakani zimepatikana, sio risasi wala sumu tena. Mapinduzi mapya kwa watawala/viongozi ni ya kikatiba ama kisheria. Rejea kuondolewa kwa Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini. Majasusi wanachezea katiba kwa mwavuli wa bunge tu inatosha kumuondoa rais madarakani. Hata hivyo, haifungi nyanja za kijasusi kutilia mkazo usalama wa viongozi duniani katika mukthada wa mauaji ya risasi kwa viongozi. Kitabu hiki kinaangazia usalama wa Rais hasa makazi ya Rais nchini Tanzania bila kuathiri itifaki na miiko mengineyo ya nchi. Mathalani, kutoka lango kuu la ikulu kwenda mpaka chumba anacholala rais (shafron)  ni mita 63.2. Hii inaonyesha kuwa Rais wa nchi hii hayuko salama hasa linapokuja suala la ulinzi wa kimitambo (artificial security), Eneo la ikulu hii ni dogo, halizidi eneo la mraba 13,200 ambacho ni kipimo kidogo kabisa kwa dunia ya leo kwakuweka makazi ya kiongozi wa nchi. Upande wa Kaskazini mita 10 kuna bahari yenye kina cha mita 18 hadi 33, hii inaweza kuruhusu nyambizi ndogo zenye makombora ya masafa mafupi kuifikia ikulu, ulinzi wa eneo hili ni  wa kiasili au nguvu ya binadamu kiulinzi (natural security) jambo ambao linatia shaka zaidi usalama wa rais wa Tanzani katika zama mpya za kijasusi,


Upande wa mashariki mwa Ikulu kuna majengo manne yenye urefu kati ya mita 30,43 na 56 ambayo ni wizara ya ardhi, wizara ya utumishi, mnara wa kuongozea meli, na chuo cha ukarani. Katika itifaki ya kiusalama majengo haya ni hatari kubwa mno kwakuwa yapo umbali wa mita 40 hadi 160 tu, eneo hili laweza kutumiwa na walenga shabaha kuelekea ikulu, hii inatokana na sehemu kubwa ya vyumba vya shughuli za rais kuelekezwa upande huu wa mashariki.  Mlenga shabaha (Sniper) yeyote akitumia moja ya majengo ya eneo hili anaweza kumuua kiongozi/mtu aliye ndani ya bafu,choo ama chumba cha mikutano bila idara za usalama zilizo ndani ya ikulu kutambua kwa haraka mlenga shabaha huyu alipo mpaka uchunguzi wa kimaabara (carbon fire missile) ambao kimsingi huchelewa kupata jibu na mlenga shabaha atakuwa keshatokomea.

Soko la samaki Feri
Eneo hili pia lina soko la samaki ambapo kiafya ni hatari zaidi kwakuwa moshi unaotokana na ukaangaji wa samaki hujaa ikulu waweza dhani mapishi hayo yanafanyika ndani ya ikulu hiyo. Upande wa kusini mwa ikulu kuna majengo matatu marefu, Wizara ya fedha, Benk kuu na magereza, eneo hili linatazama lango la ikulu, majengo haya yapo umbali wa mita 200 na 240, japo kuwa majengo haya ni ya serikali na yanatumiwa na serikali lakini kiusalama haya hayafai kuwepo maeneo haya, ikiwa adui yeyote mlenga shabaha za mbali (sniper) atatumia majengo haya basi shabaha yake itakuwa ni nyakati za rais kuingia ama kutoka ndani ya ikulu hii ya Dar. Upande wa Magharibi lipo jengo moja ambalo ni refu linalokadiriwa kuwa na ghorofa 18, jengo hili lipo umbali wa mita 370 kutoka ndani ya ikulu hiyo, na katika upande huu wa Magharibi mwa ikulu ndiko chumba cha cha kulala rais kiliko maarufu kama DDO,

Jengo la kibiashara karibu na Ikulu
Jengo hili refu ni eneo la kibiashara na makazi ijapokuwa sehemu ya makazi ya juu kabisa ya ghorofa yamechukuliwa (yamepangishwa) kwa maafisa usalama wa serikali lakini hilo haliondoi uhatari uliopo kutokana na uwepo wa majengo haya marefu pembezoni mwa Ikulu hii, Mlenga shabaha yeyote mwenye nia mbaya na taifa hili anaweza kutumia eneo hilo kudhuru ama kuua Kitabu hiki hakiyaweki haya katika maandishi kwa lengo la kuharibu, la’hasha! Bali ni ili kuliweka taifa mahali pausalama zaidi kutokana na taifa liendako, ikumbukwe kuwa miaka michache tu iliyopita eneo hili la ikulu halikuwa na uzio kabisa na watu walikuwa wakijatiza langoni kule wakitoka feri kwenda Hospital ya Saratani. Lakini kadiri mageuzi ya nchi yanavyokwenda mambo yamebadilika sasa angalau ukifika hata getini kuna ulinzi mkali wenye kusaidiwa na mitambo (artificial security) kuliko ilivyokuwa zamani (natural security),

 Sasa Tanzania inaingia kwenye nchi zennye uchumi mkubwa kutokana na raslimali gesi iliyonayo, ambayo mpaka Desemba 2015 kiasi kilichogunduliwa kinakadiriwa kuwa na gesi yenye futi za ujazo 56.8 trilioni, kiwango hiki ni robo tatu ya gesi izalishwa Urusi, na bado utafiti zaidi unaendelea. Tanzania itakuwa mojawapo ya nchi chache za Afrika zenye gesi nyingi kwa sasa ambapo kwa kiwango kilichogunduliwa tu inauwezo wa kuihudumia Italia, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza na kukidhi mahitaji yao kwa miaka miaka kumi mbele. Mwaka 2016 Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Mhongo alinukuliwa akisema, “ ikiwa gesi iliyogunduliwa nchini Tanzania serikali ya nchi hiyo ikiandaa sera na kuzifanya kuwa kwa maaslahi ya nchi hiyo basi Tanzania itakuwa nchi yenye uchumi mkubwa kwa miaka 15 tu kuanzia 2015”, Katikati ya neema hii ya utajiri ndipo viongozi wa kitaifa huhitaji ulinzi maradufu na chuki za nje huongezeka huvyo ulinzi  ukiwa legelege tutarajie chokochoko na udukuzi kwa viongozi Tanzania toka mataifa makupe ya kimagharibi hasa CIA na M16, Kwa sasa njia mwafaka ni kuhamisha ikulu hapa ilipo na kuipeleka Dodoma ikiwa dhamira ya uhamiaji Dodoma bado ipo, lakini kama Dodoma bado ni kizungumkuti basi sehemu mujarabu na yenye uwiano mzuri wa protokali za kijasusi na kiulinzi basi ni Kigamboni.

............................................................................

Makala hii ipo katika kitabu kiitwacho "Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi" kilichoandikwa na Yericko Nyerere.

 
Share on Google+

About TANZANIA INVESTEMENT ADVENTURERS

We are an Investment Club geared to use social networks as means of sharing informations, knowledge, wisdom but more importantly reducing the cost of marketing your products by reaching so many potential customers with the lowest cost ever.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment