OFISI ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga inadaiwa
kumwandikia barua Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Mwanga kutaka taarifa
mbalimbali za kesi zinazoendeshwa mahakamani kila mwezi.
Inadaiwa ofisi hiyo iliandika barua yenye
kumbukumbu namba CAB40/229/01/25 ya Julai 8 mwaka huu kwenda kwa Hakimu
Mfawidhi wa Wilaya.
Hatu hiyo ya mkuu wa wilaya imekuja wiki mbili
baada ya Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji
Salome Kaganda kuwatahadhalisha wakuu wa wilaya nchini wawe makini katika
utendaji wao ili wasije wakaingilia mihimili mingine.
Jaji Kaganda aliyasema hayo wakati wakuu hao wa
wiala walipokula kiapo cha utumishi, Ikulu Dar es Salaam hivi karibuni.
Alisema anao uzoefu na amekuwa akipokea
malalamiko mengi yanayohusu manyanyaso na uvunjifu wa maadili unaowahusu wakuu
wa wilaya.
Jaji Kaganda pia alikemea ulevi kupita kiasi, matumizi mabaya ya madaraka na tatizo la viongozi wa umma kutumia vibaya madaraka yao kwa kuingilia mihimili mingine.
Jaji Kaganda pia alikemea ulevi kupita kiasi, matumizi mabaya ya madaraka na tatizo la viongozi wa umma kutumia vibaya madaraka yao kwa kuingilia mihimili mingine.
Barua hiyo ilitaka taarifa
mbalimbali za mahakama zikiwamo idadi ya kesi zilizopo, zilizosikilizwa
na changamoto zilizojitokeza zikiwamo za sheria, fedha na vitendea kazi.
Taarifa nyingine ni kiasi cha fedha za
mashahidi zilizopokelewa na zilichotumika kuwalipa kwa mwezi husika
ikibainisha majina na fedha.
Kwa sababu hiyo, MTANZANIA lilimtafuta
aliyewahi kuwa Msajili wa Mahakama Kuu, Jaji Francis Mutungi ambaye ni Msajili
wa Vyama vya Siasa kwa sasa kujua utaratibu wa mahakama wa kutoa taarifa zake
za uendeshaji wa kesi.
“Kuna kitu kinaitwa taarifa ya marejesho…kila
mahakama ina utaratibu wake, taarifa zinakusanywa na kupelekwa Mahakama Kuu
Kanda.
“Mahakama Kuu Kanda inakusanya taarifa za
mahakama zote na kuziwasilisha Makao Makuu ambayo ni Mahakama Kuu ya Tanzania,
Dar es Salaam.
“Kazi hizi hazihitaji
hasira, inawezekana huu ni utaratibu wake yeye huyo Mkuu wa Wilaya…wanatakiwa
kuelimishwa kazi za utawala zinaendaje.
“Kwa mazingira hayo
hakimu anaweza kujibu ovyo kwa sababu hawajibiki kwa DC.
“DC naye anataka kujua taarifa za wilaya yake
kwa sababu ofisi yake inapokea malalamiko mbalimbali yakiwamo ya kesi…kufanya
hivyo anakuwa na nia njema tu.
“Lakini ni kosa kuandika moja kwa moja kwa
Hakimu Mfawidhi, hakimu naye ni kosa kujibu ovyo.
“DC alitakiwa kuandika barua kwa msajili
akiomba hizo taarifa na msajili naye ataziomba makao makuu,”alisema.
Alisema mihimili wa mahakama na utawala
haitakiwi kuingiliana bali inatakiwa kuwasiliana.
“Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ilitakiwa kupeleka
taarifa hizo kwa Msajili ikijieleza kwamba katika wilaya hiyo wamejiwekea
utaratibu wa kupata taarifa za mahakama kupunguza malalamiko kutoka kwa
wananchi, hilo linaweza kufanyika kwa nia njema tu,”alisema Jaji Mutungi.
Pamoja na hayo, MTANZANIA lilimtafuta kwa simu
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mmbago ili atoe ufafanuzi wa barua
hiyo.
Katika majibu yake kwa simu Mmbago
alisema: “Nipe hiyo barua niione ndipo nitaweza kusema. Kwa simu siwezi
kusema ….nitumie nakala ya hiyo barua inayosema haya kwani kuna ugumu
gani?”alihoji Mmbago.
Alipotakiwa afafanue kama ofisi yake
imeanzisha utaratibu huo wa kumtaka Hakimu Mfawidhi kumpa taarifa za mahakama
wilayani kwake, aliendelea kujibu kwamba mpaka aione hiyo barua
inayodaiwa kutoka ofisini kwake ndipo ataweza kuizungumzia.
Barua hiyo iliyotoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya
ina kichwa cha habari kisemacho, Taarifa za uendeshaji wa shughuli za
mahakama ya wilaya na mahakama za mwanzo katika Wilaya ya Mwanga kwa kila
mwezi’.
Pamoja na mambo mengine barua hiyo inasema:
“Mahakama wakati mwingine inakutana na vikwazo ambavyo wananchi wa kawaida
hawawezi kuelewa kwa kuzingatia kuwa ni masuala ya sheria.
“Wakati mwingine ni masuala ya fedha au
vitendea kazi, hali hiyo huleta maswali mengi na malalamiko pasipo wao kujua.
“Kutokana na hoja hizo, ofisi ya mkuu wa wilaya
inahitaji taarifa za kila mahakama iliyopo na taarifa hizo zibainishe jina la
mahakama, jumla ya kesi zilizopo, jumla ya idadi ya kesi zilizosikilizwa na
changamoto zilizojitokeza zikiwamo za sheria, fedha na vitendea kazi.
“Taarifa nyingine ni kiasi cha fedha za
mashahidi zilizopokelewa kwa mwezi husika na kiasi cha fedha kilichotumika
kuwalipa mashahidi kwa mwezi husika kwa kubainisha majina na fedha”.
Chanzo:MTANZANIA
Chanzo:MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment