GP – Mangu
Kwako Inspekta Jenerali wa Polisi
(IGP)
Salaam,
Kwanza niwie radhi kwamba
nimelazimika kwa nafasi yako na yangu, kukiuka taratibu za kiitifaki hata
nikalazimika kuandika waraka huu kwako.
Ninafanya hivyo si kwa sababu
yoyote, bali kwa sababu tu jambo au mambo yaliyonisukuma kukukifikishia ujumbe
huu, yana uzito mkubwa na kimsingi yanaweza kuathiri mustakabali mwema wa
kitaifa.
Msingi wa waraka wangu huu ni agizo
ulilotoa wewe, Inspekta Jenerali wa Polisi la kupiga marufuku mikutano ya
hadhara ya kisiasa na maandamano ya vyama vya upinzani.
Ni bahati mbaya kwamba wakati ukitoa
maagizo hayo, nilikuwa niko nje ya nchi, ingawa kwa bahati njema, Watanzania
wenye mapenzi mema na taifa lao waliopo hapa nchini na nje, walinifikishia
taarifa juu ya agizo lako hilo.
IGP, siyo desturi yangu kuandika
waraka wa namna hii mtandaoni au kupitia vyombo vya habari, ingawa safari hii
nimelazimika kufanya hivyo ili kuweka rekodi sahihi, sambamba na kukosoa sababu
ulizotoa kuwa nyuma ya agizo lako hilo.
Wakati nikiwa natafakari kwa
mshangao agizo lako hilo, na baada ya kurejea nyumbani, nilipigwa na butwaa
zaidi niliposikia Jeshi la Polisi tena katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,
likiwazuia viongozi wetu wakuu na wa juu kitaifa kufanya mikutano ya hadhara.
Agizo hilo lilifuatiwa na tukio la
kukamatwa, kushikiliwa na kuhojiwa kwa viongozi hao, akiwamo mwenyekiti wetu wa
taifa, Freeman Mbowe(MB) huko Mwanza hivi majuzi.
Katika matukio hayo yote, Polisi
mnadai kuwa na taarifa za kiintelijensia ambazo zinazonyesha kuwapo kwa
uwezekano wa kutokea kwa vurugu kwenye mikutano hiyo ya hadhara ya vyama vya
siasa.
Madai haya ya polisi ambayo hata
wewe binafsi umepata kuyatoa awali, ulipoamua kwa sababu mnazojua ninyi
wenyewe, kuminya haki zamsingi na za kikatiba za vyama vya siasa kujumuika na
kutimiza majukumu yao ya kisiasa hayana ukweli hata kidogo.
Si hivyo tu, uzoefu wa kihistoria
unakinzana na kwenda kinyume kabisa na madai hayo, kwani yako matukio mengi
ambayo yamethibitisha kwamba mijumuiko ya wanasiasa wa vyama vya upinzani,
yakiwa momaandamano na hata mikutano imekuwa ikifanyika kwa amani.
Iko mifano mingi inayoonyesha
kwamba, tumefanya shughuli mbalimbali za kisiasa kwa maana ya maandamano na
mikutano ya hadhara kwa amani na pasipo kuwapo hata kwa ulinzi wa polisi.
Mifano ya namna hiyo ndiyo
inayosababisha baadhi yetu si tu tupingana na maagizo yanayotoa mwelekeo wa
kukandamizwa kwa uhuru wakikatiba wa vyama vya siasa vya upinzani kujumuika
bali kwenda mbali zaidi na kutilia shaka hata maagizo hayo na kuyaona kuwa na
misukumo iliyojificha nyuma ya kichaka cha ‘sababu za kiintelejensia’.
Naandika waraka huu kwako nikiamini
kwa dhati kabisa kwamba, kilekilichotokea Kenya hivi karibuni ambako mahakama
ilitupilia mbalimaagizo ya namna hii ya polisi kujaribu kuzuia haki ya kikatiba
ya vyama vya upinzani kuandamana ndicho kinachoelekea kutokea hata hapa kwetu
pia.
Si hilo tu, naamini wewe IGP
ulifuatilia kile kilichotokea Uganda siku chache tu baada ya Rais Yoweri
Museveni kutangazwa mshindi wa urais ambako chama kimoja cha siasa kiliitisha
mkutano wa hadhara na kikamwapisha Kiongozi ambaye wao wanaamini ndiye
aliyeshinda urais.
Waganda hao ambao wamekuwa wakiamini
kwamba "mgombea wanaye muunga mkono ndiye aliyeshinda japo kura zake
ziliibwa", waliruhusiwa kuandamana na kukutana kwa uhuru ingawa baadae
walikamatwa.
Ni jambo la kujifunza kwamba, Waganda
hawa hawakuzuiwa na‘kuwapo kwa taarifa za kiinteligensia’ licha ya kwamba
walishtakiwa baadae.
Tunachojifunza hapa ni mamlaka za
dola, kama lilivyo jeshi letu la polisi, kuheshimu na kulinda haki za raia na
kuepuka hatari ya vyombo vyetu kujipa dhamana ya kuwaamulia wananchi masuala
yao kwa kisingizio cha taarifa za kiintelijinsia.
Je, kwa maagizo ya namna hii,
Inspekta Jenerali Mangu na wenzako polisi mnatuonaje sisi viongozi wa upinzani?
Je, mnafikiri pamoja na uzoefu wetu
katika siasa na uongozi tunaweza tukawa mbumbumbu wa kutambua haki zetu au hata
kushindwa kujua dhamana kubwa tuliyobeba ya kuwatumikia wananchi na taifa letu?
Je, IGP Mangu na wakuu wenzako wa
Jeshi la Polisi mnapotoa maagizo ya namna hiyo hamuoni kwamba mnajenga taswira
tu kwamba, malengo yenu ni kutafuta jinsi ya kutumia magari ya upupu
yaliyoagizwa kwa pesa nyingi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana?
Je, mmeshindwa kujifunza kwamba,
kama kulikuwa hakuna vurugu kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu pamoja na kuwapo
kwa kila viashiria vilivyochochewa na taasisi za dola, wapinzani hatuna sababu
hata moja ya kuwa chanzo cha vurugu za namna hiyo?
IGP Mangu, pengine ni busara
nikakukumbusha kwamba, vyama hivihivi vya upinzani chini ya mwavuli wa UKAWA
viliwahi kuandamana kwa maelfu kutoka Buguruni yaliko makao makuu ya CUF hadi
makao makuu ya CHADEMA Kinondoni kwa amani na kwa utulivu.
Je, hukumbuki kwamba katika
maandamano hayo yaliyohusisha maelfuya wakazi wa Dar es Salaam, hakuna hata
sindano ya wananchi iliyopotea wala mtu kukwaruzwa?
Hayo na mengine mengi ndiyo ambayo
yamenifanya nitafakari sana nakukosa jibu naposikia polisi mkituzuia kwenda
vijijini kuwashukuru wananchi kwa kutuheshimu na kutupiga kura zao
Ni nini hicho kitakachoathiri amani
na utulivu? Wanachama wa vyama vipi hao ambao eti watapingana kwa sababu sisi
tumeamua kuwashukuru wananchi waliotuunga mkono kwa mamilioni?
IGP Mangu, nakuomba uyatafakari haya
na kuliangalia upya agizo lako, ambalo yumkini haliitakii mema nchi yetu.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu
Ibariki Afrika
Wako,
Edward Ngoyai Lowassa
0 comments:
Post a Comment