Bila ya shaka mmepata
habari kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuwa siku ya Jumapili
ya tarehe 11/06/2016 akiwa kanisani kwake, Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima alitoa kauli za uongo, uchochezi na uchonganishi dhidi ya
Chama cha Mapinduzi, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt John Pombe Magufuli, Viongozi wa CCM,
Watendaji wa CCM na Serikali ya Awamu ya nne.
Mchungaji Gwajima
amedai ati kwamba lipo kundi la wanaCCM wanaozunguka sehemu mbalimbali za nchi
wakishawishi wanachama na wakimshawishi Mwenyekiti wa sasa Dkt Jakaya Mrisho
Kikwete ili aendelee na Uenyekiti na kuleta hoja ya kutenganisha kofia ya
Uenyekiti wa CCM na Urais wa nchi.
Napenda kuwafahamisha
wana CCM, wapenzi wa CCM na wananchi kwa jumla kuwa madai hayo ya Mchungaji
Gwajima ni uongo mtupu na hayana hata chembe ya ukweli. Ni mambo ya uzushi na
hadithi ya kufikirika. Watu hao hawapo kwani kama wangekuwepo habari hizo
zingekwishajulikana Chamani kupitia mfumo mahiri wa usalama na maadili wa ndani
ya Chama cha Mapinduzi. Chama chenyewe kingekwishawatambua watu hao na
kuwachukulia hatua zipasazo za udhibiti na nidhamu.
Kama mambo hayo
yangekuwepo viongozi wa Chama wa Mikoa, Wilaya na Matawi waliofuatwa wangekuwa
ndiyo wa kwanza kuwafichua. Habari za namna hiyo hazijapokelewa kutoka popote
na kutoka kwa kiongozi yeyote wa Chama. Kama kweli Mchungaji Gwajima anawajua
watu hao awataje hadharani na aseme walikwenda kumuona nani, wapi na lini
kufikisha ujumbe wao huo hasi dhidi ya CCM.
Napenda kusisitiza
kuwa habari za namna hiyo hazipo katika Chama cha Mapinduzi. Kwa hakika
kinachoendelea sasa Mikoani na Wilayani ni maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum
ambapo Mwenyekiti wa CCM wa sasa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atastaafu na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph
Magufuli atachaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya. Hakuna jambo lingine.
Nafurahi kuwafahamisha
Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwamba kazi ya maandalizi ya
Mkutano Mkuu Maalum inakwenda vizuri kabisa. Shughuli hiyo inasimamiwa na Naibu
Katibu Mkuu Bara Ndugu Rajabu Luhwavi kwa niaba ya Sekretarieti ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM. Kwa mujibu wa hatua iliyofikiwa sasa Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa inaweza kukutana siku yoyote kupanga tarehe ya kufanyika kwa
Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa uhakika.
Sisi katika Chama cha
Mapinduzi hatushangazwi ingawaje tunasikitishwa na kauli za uongo, uchochezi na
uchonganishi za Mchungaji Gwajima dhidi ya Chama cha Mapinduzi. Ana chuki
iliyopitiliza dhidi ya CCM na Mwenyekiti wake. Yeye ni mtu ambae hajawahi
kuitakia mema CCM. Hata yeye mwenyewe amekiri kwenye mahubiri yake ya tarehe 11
Juni, 2016 kuwa “alitaka CCM ishindwe katika chaguzi zilizopita na ndivyo
anavyotaka iwe hivyo hata sasa, ili Chama chake cha upinzani kishinde.
Askofu Gwajima |
Mchungaji Gwajima pia
hana mapenzi na wala hamtakii mema Rais Dkt John Pombe Magufuli. Kwanza,
hakutaka ashinde uchaguzi kwani alimpigania kwa hali na mali mgombea wa UKAWA.
Pili, hataki adumu na kufanikiwa katika kazi yake ya Urais, ndiyo maana anatoa
ushauri usiokuwa na mashiko na wakihasidi dhidi ya Mheshimiwa Rais. Anamshauri
ati kwamba atoke Chama cha Mapinduzi na kuanzisha Chama chake. Kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais lazima awe mwanachama wa Chama
fulani cha siasa. Hivyo basi, Rais John Pombe Magufuli akitoka CCM anapoteza
Urais na Makamu wa Rais anakuwa Rais na CCM inaendelea kuongoza. Yeye atakuwa
hana chake. Hivyo Rais wetu atakuwa amepata au atakuwa ameharibikiwa? Huo kweli
ni ushauri wa mtu anayedai kuwa na mapenzi mema na Mheshimiwa John Magufuli? La
hasha! Huo ni ushauri wa adui yake na wala siyo wa mtu rafiki na mwenye huruma
na mapenzi na Rais wetu.
Mchungaji Gwajima
anataka kufanya “danganya toto”. Napenda kumhakikishia yeye na genge lake kuwa
“CCM hatudanganyiki na Rais Magufuli ndiyo kabisa “hadanganyiki na wala
hababaiki”. Mheshimiwa John Pombe Magufuli siyo kama Bwana fulani aliyekubali
kudanganywa na Gwajima na kudanganyika. Alitoka CCM akiamini kuwa angeshinda.
Aliyomtabiria hayakuwa na sasa yeye na wenzake wanajuta na wengi wameanza
kukimbia. Rais wetu mpendwa na Mwenyekiti wetu mtarajiwa hawezi kudanganyika
kiurahisi namna hiyo. Mheshimiwa John Pombe Magufuli ni mtu makini na mahiri.
Shabaha ya Mchungaji
Gwajima ni kutaka kuleta mfarakano ndani ya Chama cha Mapinduzi kwa
kumchonganisha Rais na Mwenyekiti wa CCM. Anachotaka ni kukidhoofisha Chama cha
Mapinduzi na kumdhoofisha Rais John Magufuli ili kupalilia Chama chake na mgombea
wake washinde uchaguzi ujao.
Napenda kusema kwa
kujiamini kuwa hilo halitatokea kamwe. Mwenyekiti Kikwete ni kada aliyelelewa
na kupikika vyema na viongozi waasisi wa Chama na Taifa. Anaelewa na kuheshimu
mila na desturi nzuri ya CCM kuunganisha kofia ya Urais na Uenyekiti. Hawezi
kwenda kinyume. Hakung’ang’ania Urais, hawezi kung’ang’ania Uenyekiti na wala
hana mpango huo.
Hali kadhalika, hata
ushauri wake wa kutaka Marais Wastaafu waondolewe kinga ili washitakiwe,
shabaha yake ni ile ile ya kutaka kuleta mfarakano baina ya Rais John Pombe
Magufuli na Marais wastaafu kwa lengo lile lile la kutaka kuleta mfarakano
ndani ya CCM na nchini. Matumaini yake ni yale yale ya kudhoofisha CCM na Rais
wake ili kunufaisha upinzani. Kamwe Rais wetu hatanasa katika mtego huo.
Kwa kweli inasikitisha
kuona Kiongozi wa dini akitumia madhabahu takatifu kusema uongo na kupanga
fitina na kupandikiza chuki katika jamii. Hatutegemei Kiongozi wa dini kuwa
hivyo. Hatukupenda kujibizana na Kiongozi wa dini lakini kwa vile ameacha ya
dini na kuingilia ya upande wetu tumelazimika kusema. Wahenga wamesema
“lisilobudi hutendwa”
Nawaomba wanaCCM na
Wananchi kupuuza uongo, uzushi na ushauri hasi wa Mchungaji Josephat Gwajima.
Christopher Ole
Sendeka.
Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi.
Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi.
0 comments:
Post a Comment