Balaa la tumbua tumbua sasa lamgeukia Rais
Magufuli.Rais sasa aombwa ajitumbue wenyewe.Ombi hilo limetolewa na Msemaji
mkuu wa kambi rasmi ya upinzani katika wizara wa Ujenzi,Uchukuzi na mawasiliano
na mbunge wa Vunjo James Fransis Mbatia alipokuwa akiwakilisha bajeti kivuli ya
wizara hiyo.
Mbatia amesema katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu,
Jakaya Kikwete, Dk. Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi – wizara ambayo inatajwa
kujaa ubadhirifu wa pesa za umma na kwamba, rais huyo ameshindwa kuchukua
hatua. Hivyo kumtaka Rais Magufuli kutumbua majipu yake wakati akiwa
kwenye wizara hiyo.Alinukuliwa akisema “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inajiuliza kama serikali ya awamu ya tano inafanya kazi yake kwa haki, uadilifu, uwazi na usawa kwa wote na hasa kwa kile kinachojulikana kama utumbuaji majipu, swali hapa ni nani amfunge paka kengele? au mkuki mtamu kwa nguruwe mchungu kwa binadamu?” amehoji Mbatia.
Hizi ni sababu tatu alizotaja
Mbatia za kumtaka Rais Magufuli ajitumbue
1.Wakala wa Barabara nchini TANROADS
aliitia hasara serikali ya zaidi ya shilingi bilioni tano
“TANROADS imebainika kuwa na utendaji mbovu kama
ambavyo mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) alivyobaini juu ya
usimamizi mbovu katika mikataba ya ujenzi wa barabaa na madaraja ambapo ilikuwa
chini ya iliyokuwa wizara ya ujenzi katika serikali ya awamu ya nne,” amesema.
“TANROADS wakati wa kipindi hicho, iliitia hasara
serikali ya jumla ya Shilingi 5,616,652,051 kutoka kwenye riba
(interest) inayoongezeka kila siku kutokana na TANROADS kuchelewa kuwalipa
wakandarasi 11.”
Hasara hiyo iligundulika kati ya kipindi cha mwaka 2012
na mwaka 2015 kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ya Hesabu za Serikali Kuu wakati wa
ukaguzi wa taarifa za fedha kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2015 iliyotolewa
mwezi Machi 2016 (Ukurasa wa 134 na 135).
2. Serikali kuruhusu matumizi
ya matairi yanayofahamika kwa jina la Super single tires ambayo yanaharibu
barabara.
“Utafiti unaonesha matairi haya (super single tyres)
yanaharibu barabara. Matairi haya yameanza kutumika takribani miaka mitano
iliyopita na mzigo uliokuwa unabebwa na matairi 24 sasa unabebwa na matairi
12,” Mbatia alisema.
“Uamuzi wa
kuruhusu matairi haya haukuwa na busara maana barabara zetu hazijabuniwa
kuhimili shinikizo la uzito (excessive
pressure) linalotokana na matairi hayo,” aliongeza.
3. Uuzwaji wa nyumba za
serikali kwa bei ya hasara hivyo kuigharimu nchi.
Katika hili Mbatia alinukuliwa akisema “Katika
muktadha huo kambi Rasmi ya Upinzani inalikumbusha Bunge kwamba,
kati ya mwaka 2002 mpaka 2004 Serikali iliuza nyumba zipatazo
7,921 na mpaka mwaka 2008 Serikali ilikuwa imejenga nyumba 650 tu,”.
Amesema kuwa, katika biashara ya kuuza nyumba
zilizokuwa mali ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), serikali
ilipata Sh. 252,603,000/- ambazo haziendani na thamani halisi ya nyumba hizo.“Hivi sasa serikali inahitaji kusaka nyumba zaidi ya mara dufu ya kiasi hicho kujenga nyumba za fidia”.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya
Bunge juu ya uuzaji wa nyumba za serikali kinyume cha taratibu, serikali
itatumia Sh. 677,606,000/- kujenga nyumba mpya ili zirejeshwe kwa Tamisemi,
Rejea taarifa ya Serikali Bungeni tarehe 25 April 2008,” Mbatia alinukuliwa.
“Kumbukumbu za
taarifa rasmi za Bunge zinaonesha kwamba, serikali ilitoa taarifa ndani ya
Bunge hili kuwa, kuna kamati iliundwa kuchunguza mchakato wa mauzo ya nyumba ya
serikali”.“Kamati hiyo ilitegemewa kumaliza kazi mwezi Februari, 2007, lakini hadi Bunge la Tisa na Bunge la Kumi linamaliza uhai wake hakuna taarifa iliyotolewa na serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani Buneni inaitaka serikali ya awamu ya tano irejeshe nyumba hizo,” amesema.
Mbatia alimalizia kwa kusema Rais Kikwete alitoa agizo nyumba hizo zirudishwe lakini Rais Magufuli akiwa waziri alishindwa. “Tukumbuke kuwa Rais Kikwete alielekeza nyumba hizo zirudishwe serikalini lakini alikosa uthubutu wa kusimamia kauli yake,” amesema
0 comments:
Post a Comment