ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajabu Rutengwe, amezua tafrani
katika Kijiji cha Mboga kilichopo Msoga mkoani Pwani  baada ya kuzuia
mradi wa Kiwanda cha Matunda cha Sayona kisijengwe mpaka alipwe fidia ya Sh
milioni 150.
Dk. Rutengwe anataka alipwe  fidia hiyo kwa ajili ya kupitisha
nguzo za umeme katika shamba lake pamoja na barabara inayochongwa mbele ya
shamba hilo.
Alisema kamwe bila malipo hayo mradi huo utasimama.
Hali hiyo imewafanya wakazi wa kijiji hicho kumjia juu Dk. Rutengwe
wakisema wao wanataka kiwanda ambacho kitawasaidia kukuza uchumi wao na vijana
kupata ajira.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara  uliofanyika juzi kijijini
hapo kwa ajili ya zuio la mradi wa umeme na barabara  unaotakiwa kwenda
kiwandani hapo, Diwani wa Kata ya Msoga, Hassan Mwinyikondo (CCM), alisema Dk.
Rutengwe ameliandikia barua Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Pwani,
akilitaka lisipeleke nguzo za umeme eneo hilo ambako kiwanda kinatarajia
kujengwa hadi alipwe fidia.
Alisema baada ya kupata malalamiko ya Dk. Rutengwe, alilazimika kukutana
na halmashauri ya kijiji hicho ambako wajumbe walikiri kumtambua mwekezaji huyo
kutokana na kufuata taratibu zote.
“Namshangaa Dk. Rutengwe, maana yeye ni mzaliwa wa hapa halafu leo
anakataa kijiji chetu kisipate kiwanda, tunaamini  kiwanda hiki kina
manufaa kwa wananchi wetu… siwezi kumvumilia maana anakwamisha maendeleo ya
kijiji na wananchi kwa ujumla,” alisema Mwinyikondo.
Alisema wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, alikwenda kijijini hapo
na kupitisha nguzo za umeme na bomba la maji  katika mashamba ya watu,
lakini hakuna fidia aliyodaiwa, sasa iweje sasa hivi sasa azue mgogoro wa aina
hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Jijiji hicho, Rashid Hemed, alisema wamejaribu
kumwelimisha Dk. Rutengwe kuwa barabara hiyo ni mali ya Serikali kwa sababu
ilikuwa ikitumika tangu enzi za ukoloni kusafirishia mizigo yao, bado
alikataa  kwa kumwandikia barua ofisa mtendaji wa kata na Tanesco
wasimamishe mradi huo.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Idd Hulela, aliyezaliwa mwaka 1933
alisema barabara anayoitaka Dk. Rutengwe ni mali ya Serikali tangu enzi hizo.
Meneja Mradi  wa kiwanda hicho kutoka Kampuni ya Sayona, Aboubakary
Mlawa, alisema ujenzi wa kiwanda umepitia hatua zote, mbali na barua hizo, Dk.
Rutengwe amekuwa akimtumia ujumbe kwa njia ya simu ya kiganjani akimtaka
asimamishe mradi huo.
Alisema kama kiwanda hicho kitakamilika kitaajiri Watanzania 800 hatua
ambayo itasaidia kupunguza tatizo la ajira.
Kwa upande wake mwakilishi wa Dk. Rutengwe, Said Hemed, alisema 
bosi wake  hataki tena fidia hiyo.
Alisema naye anataka mradi huo uendelee kufanyika  wananchi wapate
maendeleo, lakini alitaka haki itendeke kwa wananchi waliopo kijijini hapo.
(Habari hii ni kwa msaada wa
gazeti la Mtanzania)
 

0 comments:
Post a Comment