Je Wajua Kuwa Uchawi Na Miujiza Ni Mapacha?


 
 
Na: Dotto Rangimoto Chamchuwa
 
UCHAWI na MUUJIZA ni masuala tata katika jamii, pamoja na utata wake lakini yamekuwa ni masuala ya kawaida kusikika. Ni kawaida kusikia fulani ni mchawi au nimefanyiwa uchawi. Pia ni kawaida kusikia kuwa fulani ana miujiza au nimefanyiwa miujiza. Uchawi ni nini? Muujiza ni nini? Ipi tafauti kati ya uchawi na muujiza?

Kwanza kabisa naomba nikiri mapema kuwa, mambo haya ni ya kiimani zaidi. Kwakuwa ni ya kiimani, na mimi ufafanuzi wangu utategemea rejea za imani zinazokubali uwepo wa uchawi na muujiza, hususani toka kitabu cha qur-an na biblia.

Katika dini zote, hadi zile za kipagani, zina amini kuwa ulimwengu na vilivyomo ndani yake vimeumbwa na MUNGU. Si ukweli hata kidogo kuwa mungu ni mmoja, kwani kuna watu wanasema kuwa mungu ni mmoja.

Kila dini iko na mungu wake, na kila dini inaamini kuwa mungu wake ndiye aliyeumba ulimwengu na vilivyopo ndani ya huo ulimwengu. Kwakuwa kila dini iko na mungu wake, na kwakuwa dini ziko nyingi, iweje sasa mungu awe mmoja?

“Sema: Enyi makafiri! Siabudu mnacho kiabudu; Wala nyinyi hamuabudu ninaye muabudu. Wala sitaabudu mnacho abudu. Wala nyinyi hamuabudu ninaye muabudu.  Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu.” Qur-an 109:1-6

“Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika.  Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi” Waamuzi 2:12-14

Pamoja na mambo mengine aya hizo kutoka katika qur-an na biblia zinatufunza kuwa, kuna miungu  mingi na dini ziko nyingi pia. Kila mtu anaona mungu wake yuko sahihi kuliko mungu wa mwenziwe. Jambo la kuzingatia ni hili, kwa kiwango kile ambacho mtu huona mungu wake ni sahihi, basi ni kwa kiwango hicho hicho mungu huyo huonekana na watu wengine  si lolote.

Si lengo la andishi hili kuelezea miungu na dini sanjari na uhalali wake, lakini nimelazimika kuelezea kwa kifupi ili nikija kuzungumzia masuala ya nani hasa aliyeumba ulimwengu nisiwachanganye watu.

Nataka watu wajue kuwa MUNGU ndiye aliumba ulimwengu, huyo mungu anaweza kuwa Yesu, Allah[s.w], Yehova, mzimu, mlungu, nk. Hii itategemea katika dini yako mungu wako ni nani, kama ni Yesu, basi Yesu ndiye atakayekuwa kaumba ulimwengu kwa mujibu wa imani yako, na si vinginevyo!

Mungu ameumba ulimwengu, ulimwengu ambao umegawanyika katika mapute mawili. Pute la kwanza linaundwa na maada(matter & dark matter) Pute la pili limeundwa na sheria zinazotawala hizo maada(energy & dark energy).

Ndani ya sheria za kimaumbile kuna  proglamu zinazoamrisha[command] maada zifanye yale tunayoyajua na tusiyoyajua. Cha kuzingatia ni kuwa, hizi sheria ni sehemu ya ulimwengu, na zimeumbwa makhususi ili kuzifanya maada zisikiuke matakwa ya MUNGU.
 
Upande wa maada ndio kuna (matter &dark matter), Upande wa sheria za kimaumbile ndio kuna (energy & dark energy). Vyote kwa pamoja ndio vinafanya ulimwengu.

“Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake?  Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia?” Ayubu 38:32-33

“Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote” qur-an 7:54

Hiyo “amri ” inayotajwa katika aya hizo ndio sheria za kimaumbile(energy &dark energy), yaani nguvu za mvutano na zinginezo ambazo zipo kuyaongoza magimba na nyota mbali mbali zipite katika njia ambazo zimepangiwa na zifanye mambo yaliyoamriwa kuyafanya. Sheria hizo ndizo zinazotawala maada yanayounda ulimwengu.

Hizi sheria za kimaumbile zilianza kuumbwa kabla hata ya ulimwengu kuwako. Ni vigumu sheria hizi kuvurugwa au kushindwa dhidi ya vitimbi vya waja. Mfano, mtu anapochinjwa shingo hata kichwa kitengane na kiwiliwili ni lazima huyo mtu afe, sababu sheria za kimaumbile zinazotawala mwili huamrisha[command] mwili ufe pindi ukipatwa na tukio hilo. La kuzingatia ni kuwa, kila kitu na kila  tukio hutawaliwa na sheria za kimaumbile.

Pamoja na ugumu uliopo katika kuzikiuka na kuzishinda sheria za kimaumbile haiondoi ukweli kuwa watu, majini, malaika na mungu mwenyewe wamekuwa wakizikiuka na kuzishinda sheria hizi mara nyingi tangu ziliposimikwa.
Al maarufu kama DR.Manyaunyau Mtaani
Uchawi ni nini? Uchawi ni ile hali ya kukiuka au kuzishinda sheria za kimaumbile pasina kupata kibali au ruhusa kwa mmiliki wa sheria hizo. Mmiliki wa sheria hizo Mungu. Mtu yoyote anayekiuka au kuzishinda sheria hizo katika muktadha huo huitwa MCHAWI.

Mfano mtu akichinjwa katika namna niliyoeleza hapo juu, na bado akiendelea kuwa hai huku kichwa kikilalamika kwa kitendo cha kuchinjwa, basi jua kuwa sheria za kimaumbile zimekiukwa na kushindwa kufanya kazi yake. Tukio hilo litakuwa ni uchawi endapo aliyefanikisha ukiukwaji na ushindwaji wa sheria hizo hakupewa kibali na ruhusa toka kwa Mungu.

Muujiza nini? Muujiza ni ile hali ya kukiuka au kuzishinda sheria za kimaumbile kwa kupata kibali na ruhusa toka kwa mmiliki wa sheria hizo. Tukio nililolitaja hapo juu, la mtu kuchinjwa na kisha kichwa chake kilalamike kwa kufanyiwa hivyo, utakuwa ni muujiza endapo aliyefanikisha ukiukwaji na ushindwaji wa sheria hizo alipata kibali na ruhusa toka kwa Mungu.

“Bwana akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka.  Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama Bwana alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.  Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.  Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.” Kutoka 7:10-12

“Wakasema: Ewe Musa! Je! Utatupa wewe, au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa? Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio. Basi Musa akaingia khofu nafsi yake. Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye shinda. Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyo viunda. Hakika walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo. Basi wachawi wakaangushwa wanasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa Harun na Musa! “ Qur-an 20:65-70

Aya za hapo juu toka katika qur-an na biblia zinaelezea kisa cha Firauni na Musa[a.s] kwa ufupi. Watu wa Firauni walitupa fimbo na kamba zao, kisha zikageuka kuwa nyoka. Naye Musa[a.s] akatupa fimbo yake, nayo ikawa nyoka na ikawameza wale nyoka wengine. Kitendo cha fimbo kutoka katika umbile lake na kuwa nyoka ni kitendo kilichosababishwa na ukiukaji wa sheria za kimaumbile. Kitendo hichi alipokifanya Musa[a.s] kiliitwa “MUUJIZA” na kilipofanywa na watu wa Firauni kiliitwa “UCHAWI” ingawa kimsingi tukio ni moja, na si lingine, bali ni fimbo kugeuka kuwa nyoka!

Huyu Ni Mchungaji Kanisani
Uchawi na muujiza ni watoto mapacha na wana fanana sana. Kutokana na kufanana huku ndio maana wakati mwingine watu hujikuta “uchawi” wanauita “muujiza” na “muujiza” wanauita “uchawi”, lakini ukweli uko wazi kuwa “uchawi” na “muujiza” ni vitu viwili tafauti pamoja na kufanana kwao. Aya za hapa chini kutoka katika Qur-an zinaonesha jinsi Firauni alivyoshindwa kutafautisha kati ya “uchawi” na “muujiza”. Aliuita muujiza ni uchawi. Yawezekana alishindwa kutafautisha kutokana kibli chake au ndio upeo wake wa kufikiri ulikuwa umefikia kikomo katika suala husika hata asijue ule ulikuwa ni muujiza na si uchawi.

Ama, kwa kuwa dini ya Farao haikuwa ndio ya Mussa, na kwa vyovyote vile Mungu wa Mussa hakuwa ndio Mungu wa Farao, kama ndivyo, ni sawa muujiza wa Mussa uonekane uchawi kwa Farao, na yale ya Farao mwenyewe aone muujiza.

“Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri. Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao. (Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.  Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?” Qur-an 26:32-35
Yale mambo yote yasiyoyakawaida aliyoyafanya Yesu Kristo huitwa ni “miujiza”, kwani imethibiti mara chungu nzima katika qur-an na biblia kuwa Yesu alizikiuka sheria za kimaumbile. Alikiuka sheria za kimaumbile kwa kufufua wafu, kuponya viziwi, vipofu, wagonjwa na kwa kulisha maelfu ya watu kwa chakula cha kidogo kabisa. Pia alitembea juu ya bahari pasina kuzama, hata ile saumu yake ya siku arobani bila kula hata kidogo ni muujiza pia.

“Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope”  Mathayo 14:25-27

"Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipo kutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na Taurati na Injili. Na ulipo tengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo kukinga na Wana wa Israili ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio kufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu" Qur-an 5:110

"Akasema Isa bin Maryamu: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshia chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanao ruzuku." Qur-an 5:114

"Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto." Mathayo 14:19-21


Nafikiri hadi kufikia hapa tutakuwa tushafahamu maana ya uchawi na muujiza japo kidogo, si hivyo tu tutakuwa tumeshajua jinsi uchawi na muujiza unavyotafautiana na kufanana. Sasa nataka tujue asili ya uchawi na muujiza. Asili ya uchawi na muujiza ni Mungu mwenyewe.

Tanbihi: nikizungumzia asili ya kitu fulani, jua kuwa nazungumzia muumbaji wa kitu hicho. Mungu ndiye aliyeumba “uchawi” na huo “muujiza” Uchawi na muujiza ni viumbe wa Mungu kama vilivyo viumbe vingine, kama tikikataa kuwa uchawi na mujiiza sio viumbe wa mungu, basi tukubali kuwa kuna “kitu” kingine tafauti na “MUNGU” ndio kimeumba uchawi na muujiza, jambo ambalo halikubaliki katika dini zote, yaani, hata zile za kipagani.
 
Usikose Mwendelezo Wa Makala Haya.
Share on Google+

About TANZANIA INVESTEMENT ADVENTURERS

We are an Investment Club geared to use social networks as means of sharing informations, knowledge, wisdom but more importantly reducing the cost of marketing your products by reaching so many potential customers with the lowest cost ever.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment