Nami nimetia mkono kutunga kwa ustadi juu ya mambo yanayotokea duniani juu ya dini. Najua
wengi wameandika, wamekosoa, kukaripia na kuchochea. Naandika ili kukubaliana
nao au wengine kuwapinga kabisa kabisa.
Suala la udini ambalo lipo
halijazungumzwa kwa kina haswa, mimi nitajaribu kuliandika bila ya upendeleo
kwa sababu mie si mdini, si maamuma wala si mwana zuoni wa kidini. Si mkristo
wala si muislamu. Mkristo au muislamu hata awe vipi kwa mafundisho ya dini zao
yalivyo atapendelea dini yake tu (suffer
from religious bias). Labda awe msaliti wa dini hiyo.
Kuna umuhimu mkubwa kuandika ajenda hii
ya udini kwa mintaarafu ya sio kuupinga udini tuu bali kukataa kabisa dini
hizi. Haina haja ya kulaumiana, adui wetu wa msingi ni dini hususani hizi ukristo
na uislam.
Kwa hali hio hapo juu, nikienda mbali zaidi
utaona ubaguzi wa kidini hauishii kati ya wakristo dhidi ya waislamu tu au
vyenginevyo, bali utagundua ubaguzi na
chuki za kidini zipo hata kati ya
madhehebu yanayounda dini hizo. Sote tunajua kwamba wakatoliki na
waprotestant hawaivi chungu kimoja. Waprotestanti wakijiona bora mbele za Mungu
dhidi ya wakatoliki, tunajua pia wasunni wana mgogoro wa kufa mtu dhidi ya
washia. Dini ni chanzo kikubwa minyukano ya kijamii katika historia.
Kama hivyo ndivyo, watanzania wenzangu mnapaswa
kumaizi pia, kwamba tangu kisa cha Nuhu wa Biblia na Quruani mpaka nabii Musa ni
vita vita vitah vya kidini! Tangu mfalme Daudi mpaka kuzaliwa kwake Yesu (Issa),
vita vya kidini ndivyo vilivyoongoza kumwua na kumfyeka mwanadamu usoni mwa dunia
wayahudi wakijinata na kujivunia ushindi dhidi ya mataifa.
Tangu mtume Muhammad (Sw) mpaka Othman
ni vita, ni vita na utekaji wa maeneo, watumwa na mali. Wote mazayuni na makureshi
wakijivunia ushindi dhidi ya mataifa yasio amini dini zao. Huku unaambiwa dini
ni njia maridhawa kwenda kwa Mungu.
Hata wakrito wameuana sana kwa mfano
katika dola kuu ya Rumi miaka 772AD Dola Takatifu ya Rumi chini ya mfalme Karlo
Mkuu alitumia ukristo kueneza utawala wake kwa upanga. Mnamo mwaka 782AD aliuwa
watu wasiopungua elfu nne baada ya kugundua kwama mfalme anatumia ukristo
kueneza utawala wake. Wale waliuliwa kisa walikataa kushirikiana na Karlo. Vita
vingi mno, vikiwemo vita vya msalaba kati ya wislamu na wakristo.
Migogoro ya kifalsafa iliiendelea
kulitafuna kanisa, mara hii ni mgogoro wa nafasi ya Yesu Kristo katika utatu
mtakatifu, uungu wa Yesu, ibada za kusubu sanamu. Hayo yote yalipelekea mubwa
chuki na migogoro katika kanisa.
Jambo ambalo linafikirisha zaidi ni
jinsi gani mambo yalivyowekwa na hizi dini, kwamba kwa kua tumefundishwa juu ya mamlaka ya kimungu,
tunajua kua yeye ni muweza wa yote, bwana wa majeshi na mwenye enzi, basi
ilipaswa yeye atupiganie sisi kwa kua
sisi binadamu ni dhaifu laisa kiasi. Kinyume chake sisi tunampigania yeye, tena
kwa kuuana ni ngumu sana kuelewa! Hakuna mafundisho mengine ya kidini zaidi ya
haya?
Je kama banaisraeli wameuana na majirani
zao waarabu miaka na kaka hadi sasa naandika makala haya, sisi tutashindwa?
Ikiwa waarabu wamepigana vita ambavyo vimebatizwa “utukufu” na hapa ni wote
(banaisraeli, wakristo na waislamu), je kuna vita vitatakatifu kweli? Sisi
watanzania maamuma tutapona? Kama vita
hivi ni vya kidini raia hawabakwi, hawalawitiwi, na mali haziibwi? Ndio dini
hiyo?
Hivi minyukano hii ni ya kidini au
kinyang’anyiro cha rasilimali? (scramble
for scarce resource). Mimi nimewasikiliza sana mashehe na wana harakati wa
kiislamu je wanazo hoja? Na wakristo pia? Najua hoja za dini zote ni kwamba
zinaonewa. Katika fursa za kielimu, kisheria, ajira na kiutawala. Nasema hivvyo
huku nikikumbuka wakati tunamaliza A-level mimi na rafiki yangu, aliomba tempo
kwenye kampuni fulani hapa Zanzibar majibu aliyopewa yanatia kinyaa aliambiwa
vyeti vizuri ila jina lake bayahhh! Alikuwa na jina la kikristo liliolambatana
na kisukuma. Alikosa kazi rafiki yangu yule.
Najua wenye majina ya kislaamu wanakosa kazi pia kwanye taasisi
zinazoongozwa na wakristo. Inakirihisha.
Ushauri wa bure, na hapa ni kwa waumini
kwani wao ndio watakaoumia zaidi katika vita vya kidini. Wakigundua kwamba hizi
dini tunazogombania sio jambo asilia la kimungu na hakuna uhusiano wowote na
Mungu basi hatutagombana na viongozi watakosa watu wao kuwapiganisha.
Tukijua kua dini hizi ni njia tu ya
maisha hatutauana, tukijua tena dini zililetwa na wakoloni wakizungu na waarabu
kwa nia ya kututawala hatutagombana. Tukitambua kuwa dini ni mithili ya katiba hatuna
sababu ya minyukano. Tukiwa na katiba nzuri hatuna haja ya dini. Ndugu wananchi
tukimmaizi adui dini tutabakiwa na maadui watatu wakubwa rushwa, umaskini na
ujinga. Mababu zetu waliishi miaka nenda rudi bila ya dini hizi, hivi walikua
heyawani wale?
Dini si chanda chema, sio ukristo wala
si uislamu tu! Hapa kwetu tuna makabila mengi na kila kabila lina dini yake, hizo
pia si mali kitu seuze dini hizi mbili. Waafrika bwana! Hata huko ulaya na
arabuni dini zimekwenda harijojo, hazipo tena, imekua ni utamaduni tuu. Mungu
yupo na ataendea kua Mungu basi, yeye ni mtukufu hahusiani na madhaifu yetu na
dini zetu. Hata iweje wenye dini ndio
makahaba, abracdrakla, mafisadi, wauaji, waongo wanfik mashoga na walawiti. Kwa
nini bado tunasumbuliwa na ukimwi kama dini ni msaada?
Sisi watanzania tutauana kwa misingi ya
kidini kama mataifa mengine tusipolimaliza jambo hili au mnadhani sisi ni wema
sana, tuna akili kuliko Somalia, Syria, Nigeria.nk. Hii mitafaruku
inasababishwa na dini zenyewe kwa sababu ya utata wake (ambiguous philosophy). Kila dhehebu na tafsiri yake mwisho wake
vita. Haisemwi ni nani mwenye tafsiri ya mwisho kutafsiri mafunzo hayo.Mambo ni
shaghala baghala. Huo ndo ukweli.
Natabaruk makala haya, kwa kisa
kilichonitokea mimi mwenyewe hapa mjini Zanzibar nikiwa najikongoja kuelekea nyumbani,
mara akatokea rafiki yangu muuza dagaa, mpiga domo kwenye siasa za hapa Zanzibar,
na hasa mpinga muungano. Mwenye maoni hasi juu ya wabara na wazanzibara kwa
ujumla. Alinijia na kunihubiri mara hii, akiniambia nisilimu lau sivyo
nitapelekwa motoni siku ya kiama. Nikamjibu nikisilimu nitapata nini? Nitakuwa
na tofauti gani na wasilamu au wakristo? Nikamwambia mimi si muislamu wala si
mkristo, nina makosa, sina dhambi. Sisilimu wala Siritadi!!!
Na: Samson Kibona (Atheist)
Wasallam.
0 comments:
Post a Comment