UTAJIRI WA CONGO, LAANA KWA WENYEJI, NEEMA KWA WAGENI.

Dr. Christopher Cyrilo.

(Kwa msaada wa Mtandao, vitabu vya historia, majarida, makala na habari.)

Mwaka 1964, Baba wa Taifa la China, mwanamapinduzi mkomunisti Mao Tse Tung alijisemea, Tukiichukukua Congo tumeichukua Africa yote. Lakini pia katika kitabu chake, Hearts of Darkness cha mwaka 1889, Joseph Conrad anaandika, 'Congo inapaswa kuwa moja kati ya mataifa tajiri duniani'. Hata leo Congo ni nchi tajiri kuliko hata watu mashuhuri wa zamani walivyo dhani.

UTAJIRI WA CONGO.
  1. Asilimia 80 ya ardhi ya Congo inafaa kwa kilimo, ni nchi yenye eneo kubwa sawa na Ulaya Magharibi. (England, France, Germany, Italy, Netherland, Spain, Portugal, Belgium, Austria, nk.)
  2. Congo ina hazina ya asilimia 10 ya shaba ya dunia nzima. Asilimia 30 ya cobalt ya dunia nzima, dhahabu, Almasi, Platinum, Bauxite, Lead (risasi), madini ya fedha, Zink, na inazalisha asilimia 80 ya madini ya Coltan yanayotumika kutengenezwa Simu, Sumaku, iPods, na injini za 'Jet'. Congo pia ni tajiri kwa Uranium. Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia, Marekani waliipiga miji miwili ya Japan kwa mabomu ya atomic, Hiroshima na Nagasaki. Mabomu yale yalitengenezwa kwa madini ya Uranium iliyoibwa Congo.
  3. Mto Congo ni mto wa pili kwa Ukubwa duniani, una maporomoko (Inga water falls) yanayoweza kuzalisha umeme na kusambazwa Africa na Ulaya kwa Pamoja.
  4. Kuna aina 1100 za madini katika nchi yote ya Congo, Utajiri wa madini peke yake unakaribia dola trilioni 24, sawa na uchumi wa marekani na Ulaya kwa Pamoja.
  5. Mafuta ambayo bado kuchimbwa, Misitu, wanyama, vivutio vya utalii, mito na mabonde yenye unyevu na rutuba, maziwa, bahari, nk.
  6. Miaka ya 1890s, wakati wa ugunduzi wa Rubber iliyotumika kutengeneza mifuko, matairi ya baiskeli, pikipiki na magari, Congo ilikuwa mzalishaji mkuu katika dunia. Leo haipo kwenye orodha.

Leo hii, Miaka 126 baada ya mwandishi Joseph Conrad kuitabiria Congo kuwa moja kati ya mataifa tajiri duniani, bado ni moja kati ya mataifa madogo na masikini wa kutupwa duniani. Ikiwa na idadi ya Raia milioni 75, asilimia 80 ya Raia wake, sawa na raia 60 milioni wanaishi kwa chini ya dola moja kwa siku.

Wageni kutoka nje na ndani ya Africa wameivamia Congo, kusababisha machafuko, kuvuruga utaratibu wa kiuchumi na kuiba mali za Congo, kuiacha hohehahe. Mataifa ya Magharibi ndio yanahusishwa kwa kiasi kikubwa kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, kufadhili vikosi vya waasi kwa idadi isiyohesabika,  kukwapua madini na kuzinufaisha nchi hizo. Haitoshi, matatizo hayo hayaripotiwi kwenye vyombo vya habari vya magharibi isipokuwa tu pale maslahi yao yanapokuwa hatarini.

Kwa mfano, inadaiwa kuwa Kikosi cha waasi wa M23 kinafanya kazi kwa maelekezo ya serikali ya Rwanda na kimefanikiwa kwa kiasi kuinua uchumi wa Rwanda kwa kudhibiti maeneo kadhaa ya machimbo ya madini, hofu ya mataifa makubwa juu ya M23 kutishia maslahi yao ndio iliyopelekea kuwatumia marais wa Africa kusini, Jacob Zuma na Tanzania, Jakaya Kikwete kutumiwa kwa mgongo wa AU, kupeleka majeshi yao Congo kupambana na M23 tu wakati kuna vikosi lukuki vinavyofadhiliwa na kupewa silaha kutoka magharibi. 

Hapa, ikiwa ni kweli, basi viongozi hao wa Tanzania na Africa Kusini wanaingia katika historia chafu ya kusaidia upande mmoja unaoibia Congo kwa kisingizio cha kutunza Amani. Yawezekana pia walikuwa na maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya Congo na mataifa yao.

Ni Michezo ya Mataifa ya Magharibi. Wakati majarida na televisheni za ulaya na marekani zikisheheni habari za Darful Somalia, huko Congo vifo vinatokea kwa kasi ya Mara kumi kuliko ile ya Darful. Kutoka mwaka 1998 hadi 2014, raia milioni 5.5 wamekufa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, hasa kwenye maeneo yenye machimbo madini. Huo ni wastani wa vifo 941 kwa siku, lakini sio habari kubwa. Kwa maana nyingine ni kwamba, kuanzia mwaka 1998, kila siku kuna vifo vya idadi ya watu karibu sawa na ajali ya MV Bukoba, kila siku hadi mwaka 2014, kwa sababu vita tu.

Ni machafuko pekee ndio yanaweza kuifanya Congo kubaki kuwa  nchi tajiri lakini Taifa masikini, huku ikiendela kuyatajirisha mataifa ya Magharibi na majirani zake wanaoitumia vizuri.

WAKOLONI WA CONGO WAMECHANGIA.
Mfalme Leopold II, kiongozi mbabe wa kibelgiji, aliyeitawala kwa muda mrefu kuliko wafalme wote, 1865 -1908, ndiye anayetajwa kuanzisha madhara haya yanayoendelea hadi leo. Wakati wa utawala wake kikoloni waCongo walitaabishwa kwa kazi ngumu, vipigo, uonevu na malipo haba. Huku mfalme Leopold II na wabelgiji wengine  wakistarehe katika kasri yake ndani ya jiji la Leopoldville, leo hii Kinshasa. Aliweza pia kupanda farasi na vijakazi wa kiCongo kisha kwenda kustarehe huko Stanleyville, au Lubumbashi ya leo. Hata baada ya kufa kwake mwaka 1908, mfalme Albert I aliyemrithi aliendeleza ubabae wa kikoloni na uporaji wa rasilimali za Congo kwa faida ya ubelgiji na Ulaya. 

Patrice Emilio Lumumba, waziri mkuu wa kwanza wa CONGO aliyechaguliwa na wananchi mwaka 1960 hakusita kumtaja mfalme wa kibelgiji kama chanzo cha mateso na umasikini wa watu wa CONGO. Katika hotuba yake, alionesha mwanga mpya, nuru itakayoangaza Congo yote, kurejesha Amani na utajiri mikononi mwa wazawa. Hata hivyo ujasiri wa Lumumba, The African Hero, ulipelekea kuchukiwa na wakoloni na vibaraka wao, akina Joseph Mobutu. Akauawa kikatili January ya Tar.17 mwaka 1961na baadae Joseph Mobutu kujipachika Urais, na kuwa dikteta mjinga kuwahi kutoka kwenye uso wa dunia. Hadi leo hii, ardhi ya Congo bado imebarikiwa lakini Raia wake wamelaaniwa. Magonjwa, vita, umasikini na uhalifu ndio mkate wa kila siku wananchi wa CONGO, hali utajiri wao unajenga Ulaya na Marekani. 

NANI WA KUIOKOA CONGO? JE TANZANIA TULIAMUA KUGAWA RASILIMALI ZETU BILA MACHAFUKO?


Share on Google+

About TANZANIA INVESTEMENT ADVENTURERS

We are an Investment Club geared to use social networks as means of sharing informations, knowledge, wisdom but more importantly reducing the cost of marketing your products by reaching so many potential customers with the lowest cost ever.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment