NI biashara haramu ya unga, ndivyo tunavyoweza
kusema baada ya kijana Mtanzania aliyejitambulisha kwa jina la Adamu Akida,
mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam kudai kutekwa nyara na kundi la
maharamia nchini Pakistan.
Katika kile kinachoonekana kuwa ni dhuluma za
kibiashara, inadaiwa kuwa Adamu alichukuliwa na mfanyabiashara mmoja
anayejihusisha na biashara ya mihadarati, aliyemtaja kwa jina moja la Juma
mkazi wa Kunduchi Dar es Salaam na kumweka rehani kwa maharamia hao, kwa ahadi
kwamba angemfuata baada ya kumalizana nao kibiashara.
Taarifa zilizopatikana kwa watu wa karibu na
Adamu waishio Dar es Salaam, walisema kijana huyo alikwenda na
mfanyabiashara huyo nchini humo, lakini baadaye alimwacha katika mikono ya
maharamia hao kama dhamana ili baadaye awapelekee fedha zao.
Akitoa maelezo yake kwenye video ya sekunde 33
ambayo ilianza kusambaa juzi katika mitandao ya kijamii, Adamu anasikika
akiomba msaada huku watu waliokuwa wamevalia mavazi ya ‘kininja’ wakiwa wamemshikia
mitutu ya bunduki upande wa kushoto na kulia. Katika video hiyo, kijana huyo
alipofika katika eneo la kuanza kutaja mahali alipo watu hao walianza
kumshambulia kwa mateke na ngumi, huku wakiahidi kutoa video nyingine ikionesha
akiwa anachinjwa, iwapo fedha hazitatumwa.
Katika maelezo yake mafupi, Adamu alisema yupo
Garita nchini Pakistani ambako aliachwa kama dhamana na mfanyabiashara huyo
ambaye ni mkazi wa Kunduchi, jijini Dar es Salaam.Kijana huyo alisikika katika
video hiyo akitaja majina ya wazazi wake na eneo wanaloishi jijini Dar es
Salaam pamoja na jina la mtu huyo aliyemweka rehani ughaibuni.
“Nakaa Magomeni Mtaa wa Idrisa na Chemchem,
Mama yangu anaitwa Rukia Daudi na baba yangu anaitwa Akida namwomba Juma ambaye
mama yake anaitwa Mariamu alipe hela za watu kaniweka ‘Gerenta’ huku Juma
anakaa Kunduchi,” alisikika kijana huyo akisema katika video hiyo huku watu hao
wakimpiga alipoanza kutaja eneo alipo.
MTANZANIA yafika nyumbani kwao
Kutokana na video hiyo, gazeti hili lilifanya
uchunguzi ili kubaini ukweli wa tukio hilo, ambapo lilifika Magomeni nyumbani
kwao na Adamu na kukutana na mmoja wa ndugu zake ambaye alithibitisha taarifa
hizo.
MTANZANIA lilifika Mtaa wa Idrisa na Chemchem
nyumba namba 3 Kata ya Magomeni Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es
Salaam, ambapo majirani wa wazazi wa Adamu walisema wazazi wa kijana huyo
wamehama na kumwacha baba yake mdogo aliyefahamika kwa jina la Kessy Baharia.
Baada ya kubisha hodi katika nyumba hiyo
alitoka mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Khadija Katundu, ambaye ni mke
wa Baharia. Baada ya kuulizwa kama anamfahamu Adam ambaye ametekwa nchini
Pakistani, Khadija alikiri kumfahamu na kusema kuwa ni mtoto wa shemeji yake,
Akida (baba wa Adamu).
Mama huyo alisema, kwa sasa mzee Akida haishi
katika nyumba hiyo kwani alishaiuza na kuhamia Bagamoyo mkoani Pwani. “Hapa ni
nyumbani kwao Adamu kwa sababu alizaliwa hapa na kukulia hapa, lakini baadaye
nyumba hii iliuzwa na aliyenunua ni baba yake mdogo ambaye ndiye mume wangu,”
alisema Khadija.
Maisha yake
Alipoulizwa wanapoishi wazazi na ndugu wa
kijana huyo alisema baada ya nyumba hiyo kuuzwa uliibuka mgogoro baina ya ndugu
hao na kusababisha wazazi wa kijana huyo kuondoka bila kuaga na kwamba hawana mawasiliano
hadi sasa zaidi ya kusikia kuwa walihamia Bagamoyo.
Kuhusu anavyomfahamu Adamu, Khadija alisema
kijana huyo ni kinyozi na ana mke na watoto wawili ambao walikuwa wanaishi
bonde la Mkwajuni ambalo hivi sasa nyumba katika eneo hilo zimebomolewa, hivyo
kwa sasa hajui mahali wanapoishi.
Polisi wafika
Taarifa za mkanda huo wa video zimelishtua
Jeshi la Polisi ambapo tayari askari polisi jana walifika katika nyumba hiyo na
kumuhoji mama huyo kuhusu Adamu na kumwonyesha video hiyo. “Nilikuwa nasikia tu
lakini sikuamini sana lakini leo (jana) askari walifika hapa na kunihoji na
wakanionyesha video hiyo ndiyo nikaamini kuwa ni kweli Adamu ametekwa,”
alisema Khadija.Kuhusu watu waliotajwa na kijana huyo kwa jina la Juma na
mama yake Mariamu, alisema hawafahamu watu hao.
Akielezea hisia zake baada ya kupata taarifa za
kijana huyo alisema anasikitika sana na kwamba kijana huyo yupo katika hatari
ya kuuawa kama suala hilo halitapewa uzito na kufuatiliwa kwa kina.
“Kwakweli nimeshtushwa sana na taarifa hiyo na
nilivyomwona Adamu yupo katika hatari ya kuuliwa kama hatofuatiliwa lakini
naamini kwa sababu suala hili limekwisha enea dunia nzima ufumbuzi wake
utapatikana na wazazi wake watajulikana walipo,” alisema Khadija.
MTANZANIA ilipomtafuta Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine
Mahiga, hakupatina. Hata hivyo mmoja wa maofisa wa Kitengo cha Habari
katika wizara hiyo, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwani yupo likizo.
“Mimi niko likizo na leo ni ‘wekiend’ (mwisho
wa wiki) binafsi siwezi kulisemea suala hilo sina taarifa rasmi juu ya suala
hilo,” alisema ofisa huyo ambaye aliomba asitajwe jina lake gazetini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu
Nchemba hakupatikana kwani simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokewa na
baadaye alituma ujumbe mfupi wa simu kwamba yupo kikaoni.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ili kutoa
ufafanuzi kuhusu suala hilo hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Source:Mtanzania
Source:Mtanzania
0 comments:
Post a Comment