Aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira,
Dk. Makongoro Mahanga, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na
Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Ilala.
Dk. Mahanga, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri
katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete,
alichaguliwa jana na Baraza Ushauri Mkoa wa Ilala.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa Dk. Mahanga,
alisema kuwa anawashuku wana Chadema wenzake kwa mwamini kushika nafasi hiyo ya
uongozi.
“Nawashukuru sana viongozi wa Chadema ngazi ya
jimbo la Segerea na Mkoa wa Ilala kwa kuniamini kwenye Uongozi. Baada ya
kuteuliwa na kupitishwa na Kamati Tendaji jimbo la Segerea kuwa Mjumbe wa
Kamati Tendaji ya jimbo Aprili 2016, leo (jana), wajumbe wa Baraza
la Ushauri Mkoa wa Ilala wamenichagua kwa kura za kishindo kuwa Mwenyekiti wa
Chadema Mkoa wa Ilala.
“Nawaahidi viongozi na wanachama wa Chadema
Mkoa wa Ilala uongozi uliotukuka katika kukiimarisha na kukijenga Chama chetu
katika mkoa wetu wa Ilala,” alisema Dk. Mahanga.
Agosti 2, mwaka jana Dk. Mahanga pamoja na
makada wezake 20 waliokuwa wanaCCM walitangaza kukihama chama hicho na kujiunga
na Chadema .
Wakati akitangaza kuihama CCM , Dk. Mahanga,
alisema anahamia Chadema kutokana na kutokuwepo demokrasia ya kweli.
Kwa miaka mingi Mahanga amekuwa akitajwa kama
mwanasiasa kijana ambaye ni mfuasi mkubwa wa Lowassa, na ilitazamiwa kuwa
hatabaki CCM iwapo ataangushwa katika kura za maoni za kuwania tena ubunge.
Inasemekana kuwa kwake mtiifu kwa Lowassa
kumemchongea.
“Ninatangaza rasmi kuwa kuanzia leo tarehe 2
Agosti 2015, mimi Makongoro Mahanga si mwanachama tena wa CCM na ninakusudia
kujiunga Chadema kama kitakubali kunipokea,” alisema Mahanga mbele ya wanahabari
Mahanga ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Kazi,
alitoa tamko hilo saa chache baada ya kuthibitika rasmi kuwa ameangushwa katika
kura za maoni za kutafuta mgombea wa CCM kugombea ubunge jimbo hilo.
Katika hali iliyoonesha ukubwa wa tatizo la
uchafuzi wa taratibu linalolaumiwa kukithiri ndani ya mfumo wa CCM, Mahanga
alisema amechukizwa na wizi wa kura uliofanywa wakati wa uchaguzi huo.
“Nawataka pia wanachama wengine wa CCM ambao
hawakufurahishwa na wizi wa kura uliofanyika, waungane nami kujiunga na Chadema,”
alisema mbele ya waandishi wa habari aliokutana nao nyumbani kwake, Plot
1071, Kitalu S, Segerea mwisho, Dar es Salaam.
Matokeo yaliyomuangusha Mahanga, ni muendelezo
wa vipigo vilivyowakumba viongozi maarufu wa CCM katika kura za maoni
zilizofanyika nchini kote jana, wakiwemo mawaziri serikalini.
Source:Mtanzania
0 comments:
Post a Comment