Barua Ya Wazi Ya Lowassa Kwa IGP



 
 
 
GP – Mangu

Kwako Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP)

Salaam,

Kwanza niwie radhi kwamba nimelazimika kwa nafasi yako na yangu, kukiuka taratibu za kiitifaki hata nikalazimika kuandika waraka huu kwako.

Ninafanya hivyo si kwa sababu yoyote, bali kwa sababu tu jambo au mambo yaliyonisukuma kukukifikishia ujumbe huu, yana uzito mkubwa na kimsingi yanaweza kuathiri mustakabali mwema wa kitaifa.

Msingi wa waraka wangu huu ni agizo ulilotoa wewe, Inspekta Jenerali wa Polisi la kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano ya vyama vya upinzani.

Ni bahati mbaya kwamba wakati ukitoa maagizo hayo, nilikuwa niko nje ya nchi, ingawa kwa bahati njema, Watanzania wenye mapenzi mema na taifa lao waliopo hapa nchini na nje, walinifikishia taarifa juu ya agizo lako hilo.

IGP, siyo desturi yangu kuandika waraka wa namna hii mtandaoni au kupitia vyombo vya habari, ingawa safari hii nimelazimika kufanya hivyo ili kuweka rekodi sahihi, sambamba na kukosoa sababu ulizotoa kuwa nyuma ya agizo lako hilo.

Wakati nikiwa natafakari kwa mshangao agizo lako hilo, na baada ya kurejea nyumbani, nilipigwa na butwaa zaidi niliposikia Jeshi la Polisi tena katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, likiwazuia viongozi wetu wakuu na wa juu kitaifa kufanya mikutano ya hadhara.

Agizo hilo lilifuatiwa na tukio la kukamatwa, kushikiliwa na kuhojiwa kwa viongozi hao, akiwamo mwenyekiti wetu wa taifa, Freeman Mbowe(MB) huko Mwanza hivi majuzi.

Katika matukio hayo yote, Polisi mnadai kuwa na taarifa za kiintelijensia ambazo zinazonyesha kuwapo kwa uwezekano wa kutokea kwa vurugu kwenye mikutano hiyo ya hadhara ya vyama vya siasa.

Madai haya ya polisi ambayo hata wewe binafsi umepata kuyatoa awali, ulipoamua kwa sababu mnazojua ninyi wenyewe, kuminya haki zamsingi na za kikatiba za vyama vya siasa kujumuika na kutimiza majukumu yao ya kisiasa hayana ukweli hata kidogo.

Si hivyo tu, uzoefu wa kihistoria unakinzana na kwenda kinyume kabisa na madai hayo, kwani yako matukio mengi ambayo yamethibitisha kwamba mijumuiko ya wanasiasa wa vyama vya upinzani, yakiwa momaandamano na hata mikutano imekuwa ikifanyika kwa amani.

Iko mifano mingi inayoonyesha kwamba, tumefanya shughuli mbalimbali za kisiasa kwa maana ya maandamano na mikutano ya hadhara kwa amani na pasipo kuwapo hata kwa ulinzi wa polisi.

Mifano ya namna hiyo ndiyo inayosababisha baadhi yetu si tu tupingana na maagizo yanayotoa mwelekeo wa kukandamizwa kwa uhuru wakikatiba wa vyama vya siasa vya upinzani kujumuika bali kwenda mbali zaidi na kutilia shaka hata maagizo hayo na kuyaona kuwa na misukumo iliyojificha nyuma ya kichaka cha ‘sababu za kiintelejensia’.

Naandika waraka huu kwako nikiamini kwa dhati kabisa kwamba, kilekilichotokea Kenya hivi karibuni ambako mahakama ilitupilia mbalimaagizo ya namna hii ya polisi kujaribu kuzuia haki ya kikatiba ya vyama vya upinzani kuandamana ndicho kinachoelekea kutokea hata hapa kwetu pia.

Si hilo tu, naamini wewe IGP ulifuatilia kile kilichotokea Uganda siku chache tu baada ya Rais Yoweri Museveni kutangazwa mshindi wa urais ambako chama kimoja cha siasa kiliitisha mkutano wa hadhara na kikamwapisha Kiongozi ambaye wao wanaamini ndiye aliyeshinda urais.

Waganda hao ambao wamekuwa wakiamini kwamba "mgombea wanaye muunga mkono ndiye aliyeshinda japo kura zake ziliibwa", waliruhusiwa kuandamana na kukutana kwa uhuru ingawa baadae walikamatwa.

Ni jambo la kujifunza kwamba, Waganda hawa hawakuzuiwa na‘kuwapo kwa taarifa za kiinteligensia’ licha ya kwamba walishtakiwa baadae.

Tunachojifunza hapa ni mamlaka za dola, kama lilivyo jeshi letu la polisi, kuheshimu na kulinda haki za raia na kuepuka hatari ya vyombo vyetu kujipa dhamana ya kuwaamulia wananchi masuala yao kwa kisingizio cha taarifa za kiintelijinsia.

Je, kwa maagizo ya namna hii, Inspekta Jenerali Mangu na wenzako polisi mnatuonaje sisi viongozi wa upinzani?

Je, mnafikiri pamoja na uzoefu wetu katika siasa na uongozi tunaweza tukawa mbumbumbu wa kutambua haki zetu au hata kushindwa kujua dhamana kubwa tuliyobeba ya kuwatumikia wananchi na taifa letu?

Je, IGP Mangu na wakuu wenzako wa Jeshi la Polisi mnapotoa maagizo ya namna hiyo hamuoni kwamba mnajenga taswira tu kwamba, malengo yenu ni kutafuta jinsi ya kutumia magari ya upupu yaliyoagizwa kwa pesa nyingi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana?

Je, mmeshindwa kujifunza kwamba, kama kulikuwa hakuna vurugu kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu pamoja na kuwapo kwa kila viashiria vilivyochochewa na taasisi za dola, wapinzani hatuna sababu hata moja ya kuwa chanzo cha vurugu za namna hiyo?

IGP Mangu, pengine ni busara nikakukumbusha kwamba, vyama hivihivi vya upinzani chini ya mwavuli wa UKAWA viliwahi kuandamana kwa maelfu kutoka Buguruni yaliko makao makuu ya CUF hadi makao makuu ya CHADEMA Kinondoni kwa amani na kwa utulivu.

Je, hukumbuki kwamba katika maandamano hayo yaliyohusisha maelfuya wakazi wa Dar es Salaam, hakuna hata sindano ya wananchi iliyopotea wala mtu kukwaruzwa?

Hayo na mengine mengi ndiyo ambayo yamenifanya nitafakari sana nakukosa jibu naposikia polisi mkituzuia kwenda vijijini kuwashukuru wananchi kwa kutuheshimu na kutupiga kura zao

Ni nini hicho kitakachoathiri amani na utulivu? Wanachama wa vyama vipi hao ambao eti watapingana kwa sababu sisi tumeamua kuwashukuru wananchi waliotuunga mkono kwa mamilioni?

IGP Mangu, nakuomba uyatafakari haya na kuliangalia upya agizo lako, ambalo yumkini haliitakii mema nchi yetu.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

Wako,

Edward Ngoyai Lowassa

 
Share on Google+

About TANZANIA INVESTEMENT ADVENTURERS

We are an Investment Club geared to use social networks as means of sharing informations, knowledge, wisdom but more importantly reducing the cost of marketing your products by reaching so many potential customers with the lowest cost ever.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment