“BRITISH VIRGIN ISLANDS” - Chaka la kimataifa la makampuni hewa, kufichia na kutakatisha fedha

Umewahi kusikia visiwa vinavyoitwa British Virgin Islands? Utastaajabu kuwa huu ni mkusanyiko wa visiwa vingi vidogo vidogo sana lakini vikuu vikiwa ni Tortola ambapo ndipo kuna mji mkuu wa visiwa hivi,Virgin Goda, Jost Van Dyre na Anegada. Visiwa hivi viko chini ya utawala wa Malkia Elizabeth wa Uingereza lakini wakiwa na waziri wao mkuu anaeitwa Dr. D. Orlando Smith na gavana wao John S. Duncan

Kwa sensa ya mwaka 2015 mwishoni ilionyesha jumla ya raia katika visiwa hivi ni watu33,454 yani kama ingekuwa ni Tanzania basi idadi hii ni sawa ama ndogo ukilinganisha na idadi ya wakazi wa mtaa wa Kariakoo.Japo ipo chini ya milki ya waingereza lakini asilimia 82 ya raia wake ni watu weusi wakati weupe kabisa kwa maana ya waingereza halisi ni asilimia 6.8 na waliobaki ni mchanganyiko.

Ajabu lingine ni kwamba visiwa viko chini ya milki ya waingereza lakini sarafu wanaotumia ni dola ya kimarekani hii ni kutokana na ukaribu wa kiasili uliopo kati ya visiwa hivi na vile vya US Virgin Islands hivyo hata tamaduni nyingi zimeshibana. Shughuli kuu inayoingizia kipato visiwa hivi ni Utalii ukifuatiwa na shughuli za kifedha.Mfano, inakadiriwa kuwa watalii zaidi ya milioni moja hutembelea visiwa hivi kwa mwaka.

Visiwa hivi miaka ya kuishi ya binadamu ni wastani wa miaka 78 na ni moja ya sehem nzuri duniani kuishi na kufurahi. Pamoja na vile visiwa vya US Virgin Islands huitwa pepo ya duniani. Huku hakuna magonjwa ya kuambukiza wala shida uzisikiazo mataifa mengine, Huku ni kuishi tu mpaka Mungu atakapoamua kukuchukua (Kwa wanaoamini Mungu)

Chaka la kimataifa la makampuni hewa kufichia na kutakatishia fedha
Moja ya sifa kubwa na inayosumbua akili za watu sasa hivi ni hii ya visiwa hivi kutumika kama kichaka cha matajiri,viongozi wa umma na makampuni binafsi pamoja na watu maarufu kufichia fedha zao ama kufungualia makampui hewa.Zipo skendo nyingi sana zinazohusiana na kichaka hiki. Hata wakati fulani uchumi wa dunia huyumba kutokana na shughuli zinazoendelea visiwani humu vya utakatishaji fedha “Money laundering”.

Imebainika kuwa sio watu binafsi tu hata viongozi wakubwa wa dunia wanahusika katika skendo mbali mbali zinazohusiana na utakatishaji fedha. Hata serikali baadhi za dunia hufikia kuwezesha zoezi hili na hivyo kufanya biashara hii haramu kuwa ngumu kudhibitika.

Kwanini watu hufungua makampuni hewa na akaunti za benki visiwani humu?.Ni kwasababu hakuna kodi ya aina yoyote ile inayolipwa na hivyo wataalam wanapaita “ a place of classic tax heaven”. Huku mapato yake hutokana na kodi za wafanyakazi katika mishahara yao na kodi ya ardhi kwa wakazi ambapo wengi wao ni mawakala wa utakatishaji fedha.

Tabia hii ilianza mwaka 1980 pale ilipopitishwa sheria ya kuruhusu wageni kufungua makampuni na akaunti za benki visiwani humo bure na mwaka 1994 ikapitishwa sheria ya usiri na ufaragha. Mambo hayo mawili yalipelekea mpaka kufikia mwaka jana kuna makampuni hewa na akaunti za benki zaidi ya 400,000 ambazo siyo za wakazi wa visiwa hivyo.Sheria ya usiri inasababisha hakuna taarifa yoyote unayoweza kupata juu ya akaunti yoyote ukapewa zaidi ya mmiliki tu.

Moja ya skendo kubwa kuwahi kutokea ni ile iliyovumbuliwa na kundi la waandishi wa habari wa kimarekani wa Internatinal Consortium of Investgative Journalists (ICIJ) wakisaidiana na waandishi wengine 80 kutoka nchi 46 duniani. Waandishi hawa walifanikiwa kupata “hard drive” ya kompyuta yenye ukubwa wa 260 GB iliyokuwa na mafaili zaidi ya milioni 2.5 kutoka mataifa makubwa 10. Mafaili hayo yalihusisha kampuni zaidi ya 122,000 na taarifa za watu 130,000 ambao ni wamiliki, ama wawezeshaji ama mawakala wa makampuni feki ama wamiliki wa akaunti za fedha huko. Idadi kubwa wakiwa ni kutoka China, Hong Kong, Taiwan, Singapore na Urusi.

Skendo hiyo maarufu kama Panama papers ikiwahusisha marais kama Putin wa Urusi ambapo taarifa zinaonyesha washirika wake ama yeye mwenyewe wakimiliki zaidi ya dola za kimarekani bilioni 2, Rais wa China Xi Jinping, Raisi wa Ukrane Petro Poroshenko, baba wa waziri mkuuwa sasa wa uingereza David Cameroon na mlolongo mrefu wa marais mawaziri wakuu wafanyabiashara na watu maarufu.

Alipokuwa akijibu sakata hili waziri mkuu wa visiwa hivyo kwa kiburi kabisa alisema (Kwa tafsiri isiyo ya moja kwa moja) “Tunawahakikishia wateja na wadau wetu wa Hong Kong na kote duniani kuwa hili tukio la kuvuja kwa taarifa ni la bahati mbaya. Bado tunajiamini na tutaendelea kuwatunzia siri zenu kwa ufaragha mkubwa”

Itakumbuka hata hapa Tanzania kwenye sakata la IPTL na Tegeta Escrow visiwa hivi havikuwa mbali katika uhusika wake.

Tatizo kubwa limekuwa ni sheria ya usiri katika taarifa za kifedha ndani ya visiwa hivi. Uingereza ina uwezo wa kuifuta sheria hii na hivyo kuleta uwazi katika sekta ya kifedha “financial transiparency” lakini haitaki kufanya hivyo.Swali ni kwanini?

Ni kwa vipi BVI ilitokea kuwa chaka la usiri mkuu namna hii? Kwanini imeshindikana kutoa sheria hii ya usiri?

Nani yupo nyuma ya visiwa hivi?



Share on Google+

About TANZANIA INVESTEMENT ADVENTURERS

We are an Investment Club geared to use social networks as means of sharing informations, knowledge, wisdom but more importantly reducing the cost of marketing your products by reaching so many potential customers with the lowest cost ever.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment