Mahubiri Ya Askofu Gwajima Yanapogeuka Kuwa “Issue”



 
Jana jeshi la polisi lilizingira nyumba ya Askofu wa kanisa la Ufufuko na Uzima Josephat Gwajima kwa madai ya kumtafuta kwa makosa ya kutoa kauli za kichochezi katika mahubiri yake.Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Saimon Sirro nae amekiri kuwa wanamtafuta kiongozi huyo wa kiroho kwa sababu wanayo rekodi ya sauti anayosema ni ya kwake na kwamba wanamtaka ili athibitishe.
Mara kwa mara Askofu Gwajima amekuwa akisikika katika mahubiri yake mbalimbali akikikosoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kilichopo madarakani.
Aprili 17, mwaka huu akihubiri kanisani kwake, aliuchambua utendaji kazi wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli na kusema baadhi ya wanachama wa CCM wanamchukia na kumuona kuwa ni sawa na kirusi.
“Wakati Magufuli alipotangaza kugombea, wengi walijua naye ataifuata mifumo hiyo, lakini amekuwa kinyume chao ndiyo maana wanamuona ni sawa na kirusi aliyekwenda kuharibu mipango yao…  Na ndiyo maana leo anapowabana wala rushwa, wakwepa kodi na wauza dawa za kulevya wanampinga, wanamuona hafai, mimi nasema acha aendelee kuwakanyaga hadi dunia yote ijue,” alisema.

Lakini kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana uliompa ushindi Dk. Magufuli na kuwa rais, askofu huyo alisikika akiiponda CCM na kuwataka Watanzania wamchague mgombea aliyesimamishwa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa.

Juni 11, mwaka huu alisisitiza: “Moyo wangu unasema Tanzania mpya inakuja… kwa sababu anayeileta ni Mungu kupitia watu, kwa Mungu huwa mzoga unatoa asali na mimi huwa nasema wazi hata wakati wa uchaguzi nilikuwa simpendi Magufuli wale watambaji sikieni, nilikuwa simpendi, Magufuli yeye binafsi sikuwa na tabu naye, lakini nilikuwa na tabu na ile kitu inaitwa CCM.

“Wala sikutegemea kwamba atakuwa rais na nilikuwa nasema Mungu aje mtu mpya asiyetoka CCM ndiyo maana hukuniona mahali popote nimesema hiyo kitu nzuri… mimi nasemaga kweli, naona watu wameanza kukodoa macho… kodoa vizuri, mimi sikuwa naipenda CCM, siwasemei nyinyi, nilikuwa napenda iondoke kabisa, kwanini nilisema hivyo… sababu zenyewe ni zile alizozisema
Magufuli alipoingia madarakani.”
 
 
Aliongeza: “Kwa taarifa yako tulikuwa tunamjua ni mchapakazi, lakini akiingia madarakani hili dudu hili, rafiki yangu Mbowe alisema kwamba hata malaika akishuka mbinguni ndani ya jitu hili anakuwa ibilisi. Malaika Gabriel ukimshusha pale ndani ya sekunde chache anageuka kuwa ibilisi, mtanisamehe watu mnaopenda hiyo kitu, lakini mimi ni mtumishi wa bwana huwa nasema ili watu wapone, tulikuwa tunatamani hii kitu iondoke, lakini imekuja tena.

“Bahati nzuri alichaguliwa Magufuli, ni mkali na anawashughulikia wale wale aliowachagua, hana simile, yaani anapiga tu, nikasema wiki iliyopita kama Magufuli anawachakaza kweli anatakiwa ajue wale wengine anaowachakaza waliagizwa na yule kwa sababu alikuwa anawapa maelekezo. Hatukutegemea, ameanza kufanya kazi ambayo inatupa matumaini.”

Askofu huyo alisema ameyasema hayo kwani Rais Magufuli ameingia madarakani siku 60 za mwanzoni aligundua ‘flow meter’ ilikuwa haifanyi kazi.

“Ina maana mafuta miaka mitano yaliingia nchini bila kulipiwa ushuru, aliyekuwa kwenye nafasi hiyo kwa miaka 10 hakuona, jibu likaja alikuwa kimya, inatafasiri yake ya kwanza ‘am confortable’, pili nimekuruhusu na tatu usiguse hapo ni mali yangu.

“Aliona makontena zaidi ya 2,000 yametoroka bila kulipiwa ushuru na yaliletwa hajawa rais, ilikuwaje polisi wapo na usalama wa taifa wapo, hawakuyakamata kwa sababu ni ya yule mzee.

“Amekamata watumishi hewa, yule aliyetoka alikuwa hawaoni, CCM kwa utaratibu wao Juni wanatakiwa wamkabidhi unyekiti ili awe na kofia mbili ya urais na uenyekiti, lakini nimepata taarifa zangu za kiufufuo kwamba wale waliokuwa wameleta makontena bila kulipia ushuru, wafanyakazi hewa, walioharibu ‘flow meter’ wakisimamiwa na yule babu yao, wanazunguka nchi nzima ili walete hoja kwamba Magufuli asipewe uenyekiti wa chama maana anatumbua sana kila mahali,” alisema.

Askofu huyo alimshauri Magufuli kwamba kwa kuwa CCM wanataka kumnyima uenyekiti wa chama, apeleke muswada bungeni ili aondoe kinga na rais ashtakiwe kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani.

“Ikiondolewa kinga ndiyo tutajua mwendo kasi ni wa nani, UDA alinunua nani, NIDA ilikuwa ya nani, meli iliyokamatwa na pembe za ndovu kule China ilikuwa ya nani, dawa za kulevya za nani, waachie uenyekiti wao ila ondoa kinga kisha mahakama ya mafisadi ianze nao,” alisema katika mahubiri yake.
Share on Google+

About TANZANIA INVESTEMENT ADVENTURERS

We are an Investment Club geared to use social networks as means of sharing informations, knowledge, wisdom but more importantly reducing the cost of marketing your products by reaching so many potential customers with the lowest cost ever.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment